Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Fadi Boudiyeh, mwandishi wa habari na mtaalamu wa masuala ya kimkakati kutoka Lebanon, amesisitiza kuwa; kushindwa vibaya Chama cha Republican katika uchaguzi wa hivi karibuni hakukuwa jambo la kushangaza, bali kulikuwa matokeo ya lazima na ya moja kwa moja ya sera za pupa alizozifuata Donald Trump, pamoja na hatua zake za kihatarishi alizozichukua waziwazi katika nyanja mbalimbali.
Boudiyeh amesema kuwa; dalili za kuporomoka kwa nafasi ya Chama cha Republican zilianza kujitokeza tangu serikali ya Marekani ilipochagua mkondo wa kuongeza mashinikizo ya kijeshi na kisiasa dhidi ya Iran. Amebainisha kuwa mwenendo huo wa uhasama na hatua zisizopimwa zilizofuatana nao haukuishia tu katika mipaka ya Mashariki ya Kati, bali ulitikisa uthabiti wa kijiopolitiki na kiuchumi duniani kote, ukatikisa imani ya washirika wa Marekani na kuvuruga usalama wa njia muhimu za majini.
Amefafanua kuwa; raia wa Marekani ndiye aliyekuwa wa kwanza kulipa gharama za maamuzi hayo ya kihatarishi na yenye gharama kubwa. Hii ni kwa sababu vita na matumizi ya kijeshi ya Marekani nje ya nchi yaliathiri moja kwa moja maisha yake ya kila siku, kupitia mawimbi ya mfumuko wa bei yasiyo na kifani, pamoja na kupanda bei ya mafuta, bidhaa muhimu na vyakula kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.
Mtaalamu huyo wa masuala ya kimkakati ameongeza kuwa; hali ya kutoridhika wananchi iliyokuwa ikiongezeka, pamoja na hisia za wapiga kura kwamba serikali ya Trump ilichagua kutumia rasilimali za nchi katika vita vya nje kwa gharama ya usalama wa maisha yao na uchumi wa ndani, viliwasukuma wananchi wengi kuelekea kwenye vituo vya kupigia kura ili kuwaadhibu wagombea wa Chama cha Republican. Matokeo ya uchaguzi huo yameleta hatua mpya ya kushindwa na kuhitaji chama hicho cha kihafidhina kufanya tathmini upya kwa kina.
Maoni yako